MICHAEL CARRICK ATAFAKARI HATMA YAKE KUHUSU KUENDELEA KUSAKATA KABUMBU

MTU mmoja mwenye mambo adimu katika kikosi cha Manchester United, Michael Carrick amesema atafikiria hatma yake ya kuendelea kucheza soka katika msimu ujao wa 2017-18.

Katika mahojiano maalum nyota huyo amesema kwamba anafanya utafiti kuona kwamba msimu ujao uwe wa mwisho katika soka la ushindani ama la.

Akihojiwa na Sports News HQ juzi Ijumaa, nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 amesema kwamba  umri wake umekwenda lakini miguu yake inamtaka bado acheze.

“Nimewahi kusema mara kadhaa kwamba naacha soka lakini baadae yanakuja mawazo mengine, unajua mwili una masharti yake na wakati mwingine unatakiwa kuyafuata,” amesema.

Nahodha huyo msaidizi wa Manchester United ameitumikia tyimu hiyo katika jumla ya mapambano 479 ya Ligi Kuu na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakisema kwamba umri wake unamruhusu kuendelea kucheza.

“Nimejifunza mambo mengi kutoka kwa Ryan Giggs, Paul Scholes na Garry Nevile ambao wamecheza katika klabu hii mpaka wakiwa na zaidi ya miaka 30. Nafikiri ukitaka kuonyesha thamani yako katika Man United unatakiwa kuiga mfano huo,” amesema.

Hata hivyo, kiungo huyo amesema anataka kuhakikisha anaisaidia timu yake hiyo kurejea katika mafanikio yake kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu ya EPL na kuwa katika nafasi nne bora.

“Mara zote tunaangalia mbele. Tunataka kuona kwamba tunarejea katika nafasi za juu tena,” alisema.


“Kumaliza mabingwa katika Ligi ya Europa ni njia moja kubwa ya kuturejesha katika mstari ambao siku zote tunapita. Klabu kubwa kama Man United inatakiwa kuwa mabingwa wa Ulaya,” amesema.

No comments