MPASUKO MKUBWA UNANUKIA FM ACADEMIA …Nyoshi asema kila jambo na wakati wake


Baada na Nyoshi el Sadaat kuondolewa urais wa bendi ya FM Academia huku nafasi hiyo ikichukuliwa na Patcho Mwamba, Saluti5 imehakikishiwa kuwa kuna mpasuko unanukia kwenye kundi hilo.

Jana FM Academia ilifanya mabadiliko ya uongozi kwa Patcho kuwa rais mpya wa bendi, hali ambayo haijapokelewa vyema tofauti na alivyosema msemaji bendi Kelvin Mkinga.

Wakati Kelvin Mkinga akiiambia Saluti5 kuwa mabadilikoo hayo yalipokewa kwa moyo mkunjuvufu na wanamuziki wote, habari kutoka ndani ya bendi hiyo, zimedai tayari kuna kambi mbili ndani ya FM Academia na pengine muda si mrefu bendi mpya itazaliwa.

Saluti5 ilipompigia simu Nyoshi kutaka kujua amepokeaje mabadiliko hayo, akajibu kwa kifupi sana katika mfumo wa fumbo: “Samahani niko ofisi za watu, nitakutafuta baadae ila jua kuwa kila jambo lina wakati wake”.

Mwanamuziki mmoja wa FM Academia ambaye hakutaka kutajwa jina ameiambia Saluti5 kuwa mabadiliko yaliyofanywa ni matokeo ya umbeya na fitna ziliotawala kwa muda mrefu kundini.

“Kama mmiliki wetu Martin (marehemu Kasyanju) angekuwa hai, mabadiliko haya yasingefanyika, marehemu hakuwa mtu wa kukaribisha majungu,” alisema mwanamuziki huyo.

“Nyoshi ana mapungufu yake mengi, lakini sidhani kama mema yake yanafukiwa na mapungufu yake. Sisemi kuwa Patcho hafai, ila bado Nyoshi alikuwa kiongozi sahihi,” aliongeza msanii huyo wa FM Academia.

Msanii mwingine wa FM Academia amesema yeye amefurahia mabadiliko hayo lakini akafichua kuwa kikao hakijamalizika kwa amani na kwamba uko upande ambao hakujakubaliana na maamuzi.

No comments