NGOMA SASA AMALIZANA NA YANGA SC

YANGA imeonyesha kuwa na jeuri ya kutisha baada ya kumshusha nchini mshambuliaji wake Donald Ngoma na kupoteza uvumi kwamba amesajiliwa Afrika Kusini.

Hilo linakuja kufuatia taarifa kwamba Ngoma amesajiliwa na klabu ya Polokwane City ya Afrika Kusini lakini wakati uvumi huo ukisambaa, mshambuliaji huyo alikuwa yuko njiani kuja jijini Dar es Salaam kukutana na Yanga.

Ngoma alitua juzi Jumanne usiku na kupokewa na mabosi wa Yanga akipewa ulinzi mkali kutoka uwanja wa ndege mpaka katika hoteli aliyofichwa tayari kwa mazungumzo ya kuongeza mkataba na Yanga.

Taarifa rasmi kutoka ndani ya Yanga zimesema kuwa mshambuliaji huyo akiwa njiani aliulizwa na mabosi wa Yanga ambao ndio waliomtumia tiketi ya ndege ya kuja nayo nchini ambapo alikana kusaini Polokwane na kwamba anakuja kumalizana na Yanga.

Bosi huyo alisema kwamba mbali na kukana hilo, Ngoma pia aliwakana Simba akisema hataweza kuichezea timu hiyo hata kama angeshindwana na Yanga.

Taarifa iliyo rasmi sasa, Ngoma amesaini mkataba mpya wa miaka miwili haraka Jumatano, chini ya usimamizi wa Hussein Nyika ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, kabla ya kujiandaa na kujiunga na maandalizi ya timu hiyo yanayotarajiwa kuanza kesho, mara baada ya kurejea kwa kocha mkuu, George Lwandamina.

“Tumemuuliza hata mchezaji mwenyewe hata kabla ya kufika nchini akatuambia hakuna kitu cha namna hiyo ndio maana amekubali kuja nchini kuongeza mkataba na sisi, kwahiyo wana Yanga watulie Ngoma ataendelea kuwa kijana wao.”

No comments