PATCHO MWAMBA ASEMA FM ACADEMIA IMEMSHANGAZA …awapa ‘home work’ wamiliki wa bendi


Mwimbaji Patcho Mwamba (pichani juu) ambaye ametangazwa kuwa rais mpya wa FM Academia, amesema bendi hiyo imemshangaza.

Patcho amesema kilichomshangaza katika bendi hiyo ni namna wanamuziki wenzake walivyomuamini na kukubali kwa sauti moja yeye kuwa rais mpya.

Akiongea na Saluti5, Patcho amesema wanamuziki wote (ukiondoa Nyoshi) walipiga makofi na kuunga mkono pale wamiliki wa bendi hiyo walipotangaza kuwa yeye ni rais mpya wa bendi.

Patcho anaeleza zaidi: “Tulikuwa kwenye kikao cha wanamuziki wote, wamiliki wakatangaza mabadiliko na mimi nikatajwa kuwa rais mpya wa bendi, wanamuziki wakashangilia sana.

“Sikuwahi kuwaza kuwa nina thamani kubwa kiasi kile kwa wanamuziki wenzangu, kwa hakika walinishangaza sana kwa namna walivyonikubali”.

Aidha, Patcho amewatoa hofu mashabiki wa FM Academia na kusema hakuna mpasuko unaonukia.

“Ni Nyoshi pekee aliyepinga na kusema hawezi kuongozwa na mimi, lakini wanamuziki wengine wote walifurahia uteuzi wangu,” anasimulia Patcho Mwamba.

Alipoulizwa ni nini mipango yake baada ya kutwaa cheo hicho, Patcho alisema: “Kwasasa ninachohitaji kwa wamiliki wa bendi ni wao kutuwezesha kuingia studio na kutoa nyimbo mpya sambamba na video mpya.


“Tunahitaji kutoa kazi mpya chini fikra mpya, ni juu ya wamiliki kuwezesha hilo ili mashabiki watupime na ujio wetu mpya, kabla hatujaendelea na mipango mingine”.

FM Academia ilifanya mabadiliko ya uongozi juzi katika ukumbi wa New Msasani Club ambapo Nyoshi alivuliwa cheo cha urais na nafasi yake kuchukuliwa na Patcho Mwamba, hatua ambao imepokewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa muziki.

No comments