POCHETTINO ASEMA VICTOR WANYAMA ANA UWEZO WA KUISAIDIA KLABU MSIMU HUU

KOCHA Mauricio Pochettino wa Tottenham Hotspur ni kama vile huwezi kumwambia kitu chochote juu ya kiwango cha kiungo raia wa Kenya, Victor Wanyama.

Hii ni baada ya kocha huyo kukiri kuwa katika usajili ujao wa majira ya kiangazi hafikirii kabisa kuigusa idara ya kiungo kutokana na uwezo wa “jembe” hilo la maana.

Akinukuliwa na BBC, kocha huyo alisema mchezaji huyo ana sifa, nguvu na uwezo wa kuisaidia sana klabu hiyo msimu huu.

“Ni mnyama, ninamfahamu vyema kwa sababu nilimnunua nikiwa Southampton kutoka Celtic. Ni rahisi sana kutambua sifa hizi,” alisema.

Meneja huyo alikuwa anajibu maswali kuhusu umuhimu wa Wanyama kwa klabu yake, kwenye kikao na wanahabari katika kituo cha mafunzo cha klabu hiyo London.

Pochettino raia wa Argentina alijiunga na Spur Mei 2014 kwa mkataba wa miaka mitano na Mei, mwaka huu aliongeza mkataba huo na kuahidi kusalia White Hart Lane hadi 2021.

Wanyama alitua Spur kwa dau la pauni mil 11 akitokea Southampton katika dirisha la mwezi Juni, mwaka huu.


Kabla ya kuhamia Celtic, Mkenya huyo alikuwa anachezea Germinal Beerschot ya Ubelgiji.

No comments