POVU LA BAYERN MUNICH JUU YA LEWANDOWSKI SI LA KITOTO


BAYERN MUNICH imezionya klabu pinzani kuacha kumshawishi mshambuliaji wao Robert Lewandowski, na itakayopuuza ijiandae kupata vikwazo kutoka Fifa.

Staa huyo raia wa Poland amekuwa akihusishwa na uhamisho kwenda Chelsea au Manchester United, na ripoti zinadai kuwa tayari mazungumzo ya awali kuhusu dili hilo yameanza.

Hata hivyo Bayern imetoa taarifa kukanusha madai hayo ikisema: “Robert ana mkataba na Bayern na ni hivi karibuni tu ameurefusha hadi 2021. Bayern Munich haitapoteza muda kuwaza juu ya uhamisho wa Lewandowski.

“Hakuna mazungumzo na klabu nyingine na hakutakuwa na mazungumzo na klabu yoyote. Kama klabu nyingine zitafanya makubaliano na wachezaji ambao wapo kwenye mikataba ya muda mrefu, zina hatari ya kuadhibiwa na Fifa. Wakala pia ametuthibitishia kwamba hajafanya mazungumzo yoyote ya mkataba.”

Kwa upande mwingine hali inaonekana haiko sawa kwa Lewandowski baada ya wakala wake, Maik Barthel, kuikosoa Bayern kwa kutomsaidia mteja wake kushinda kiatu cha dhahabu. Straika huyo alifunga mabao 30 msimu uliomalizika na alihitaji kufunga mara mbili katika mechi ya mwisho dhidi ya Freiburg waliyoshinda 4-1 kuweza kumpiku Pierre-Emerick Aubameyang wa Borussia Dortmund aliyeibuka kinara.

“Robert aliniambia hakupata sapoti na kwamba kocha hakumpigia simu kumsaidia katika mechi ya mwisho ili ashinde taji la mfungaji bora. Alikatishwa tamaa, sijawahi kumwona kabla. Alikuwa na matumaini kwamba timu ingeweza kumsaidia kufanikisha kwa ufanisi,” Barthel aliliambia gazeti la Kicker.

No comments