PULISIC: NIMESHINDWA KUWA NYUMBU KUWAFUATA MATS, LEWANDOWSKI MUNICH

BAYERN Munich iliweza kuwachukua Robert Lewandowski na Mats Hummels kutoka Borussia Dortmund, lakini Christian Pulisic amesema hawezi kuwa nyumbu kwa kuwafuata.

Christian Pulisic amesema kwamba ni kweli marafiki zake Robert Lewandowski, Mario Gotze na Mats Hummels wameweza kuondoka Borussia Dortmund kwenda Bayern Munich, lakini hiyo haina maana kuwa lazima awafuate.

Pulisic amesema kwamba kwake yeye Dortmund ni mahali sahihi na kwamba anaona ni eneo ambalo ataishi kwa amani sana.

Mchezaji huyo raia wa Marekani alijiunga na miamba hao wa soka katika msimu wa 2015/16 na akafunga mabao matano na kusaidia mengine 13 katika mechi 43.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 amesema kwamba anataka kubaki katika kikosi hicho ingawaje pia amekuwa akihusishwa na kuhamia katika miamba hao wa Bayern Munich.

Liverpool pia walihusishwa kumchukua mchezaji huyo katika msimu uliopita, lakini mipango hiyo ilikataliwa na Dortmund.

“Naomba waniache nibaki hapa. Nataka kuendelea kubaki katika klabu hii na kwangu mimi ni mahali ambako najivunia sana,” amesema.


Mchezaji huyo amesema kuwa kwa sasa hana mipango ya kuhamia katika Ligi nyingine ikiwemo ile ya England ambako amekuwa akiwindwa sana na Liverpool.

No comments