RIO FERDINAND ‘AMKARIBISHA’ CRISTIANO RONALDO MANCHESTER UNITED


WAKATI beki wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand akimtumia meseji Cristiano Ronaldo kumtaka arudi Old Trafford, Real Madrid wanajaribu kutuliza upepo na wanataka kuzungumza na staa huyo mara baada ya hasira zake kutulia.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Rio aliandika ‘Viva Ronaldo’, akimwalika staa huyo Mreno kurudi Old Trafford baada ya kuiambia Real Madrid kwamba anataka kuondoka, huku klabu hiyo ikishangazwa na uamuzi huo ambao haikuutarajia.

Taarifa zilizozagaa Ijumaa zimedai kuwa Ronaldo, 32, aliyeondoka Old Trafford kwenda Bernabeu mwaka 2009 kwa dau la pauni milioni 80 lililoweka rekodi ya dunia, ameiambia miamba hiyo ya La Liga kwamba amechukua uamuzi ‘usioweza kubadilika’ wa kuondoka baada ya kutuhumiwa kukwepa kulipa kodi.

Tayari Jorge Mendes – wakala wa Cristiano Ronaldo amefanya mazungumzo ya dharura na Real Madrid Ijumaa na kuwaambia kuwa staa huyo ana ofa kutoka klabu za Premier League, Ligue 1 na China.

Kwa mujibu wa kituo cha redio cha COPE cha Hispania, Mendes aliwaambia mabosi wa Madrid kwamba Ronaldo amekasirishwa na tuhuma za ukwepeji kodi zinazomkabli na kwamba anahisi kutendewa kama mtu aliyefanya makosa ya jinai.


Ronaldo ambaye ameifungia Real Madrid mabao 404 katika michezo 393 tangu alipotua Benabeu mwaka 2009, anatuhumiwa kukwepa kodi ya pauni milioni 13 kati ya mwaka 2011 na 2014.

No comments