SAFARI YA MORATA KWENDA MANCHESTER UNITED YAFIKIA PATAMU …Real Madrid yatoa tamko


REAL MADRID wamewaambia Manchester United kwamba kama kweli wanataka saini ya straika wao Alvaro Morata kiangazi hiki, basi waweke mezani pauni milioni 79.

Kwa mujibu wa gazeti la Marca, Real Madrid haina haraka ya kumpiga bei straika huyo wa miaka 24 na imeiweka wazi United, kwamba haitamruhusu kujiunga nao kama watalipa fedha chini ya kiwango hicho.

Uongozi wa Madrid unajua kuwa hawana sababu ya kumuuza Morata, na Zinedine Zidane ameridhishwa na mchango wa staa huyo wa kimataifa wa Hispania aliyefunga mabao 20 katika mashindano yote msimu uliomalizika.

Jose Mourinho amemfanya Morata lengo lake kuu la usajili katika nafasi ya ushambuliaji katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi na Madrid inalifahamu fika jambo hilo.

Mwishoni mwa wiki, Marca pia liliripoti kwamba Mourinho alijaribu kumshawishi Morata akimuahidi kuwa atakuwa sehemu muhimu katika kikosi chake Old Trafford.

Inaeleweka Morata anafurahia maisha Madrid, lakini wasiwasi wake ni kwamba kukosa muda wa kucheza kutazuia nafasi yake ya kuanza katika kikosi cha Hispania wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwakani.

Alipoulizwa na gazeti la Calciomercato Jumatatu kuhusu ofa ya United, wakala wa straika huyo, Juanma Lopez alisema: “Ni klabu yenye mengi mazuri, ni chaguo linalovutia sana. Naweza kusema kwamba kuna ofa muhimu sana na uamuzi sasa unabaki kwa Real.”

No comments