SANCHEZ MGUU NDANI MGUU NJE ARSENAL

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Chile anayecheza soka katika klabu ya Arsenal ya Uingereza, Alexis Sanchez ameshindwa kuweka bayana kama anabaki kwenye klabu hiyo au anaondoka.

Sanchez ni mmoja wa wachezaji wanaotawala vichwa vya habari kwa sasa na mashabiki wa timu hiyo hawana uhakika kama atabaki katika kikosi cha kocha Arsene Wenger.

Hata hivyo mwanasoka huyo amesema kwamba anaweza kubaki ama kuondoka katika klabu hiyo na inategemea sana na matakwa ya wakala wake na namna mambo yanavyokwenda.

Sanchez ameibuka na kuyasema hayo baada ya ukimya wa muda mrefu huku akihusishwa kuhamia timu mbalimbali ikiwemo Chelsea.

“Naangalia ambacho wakala wangu anakifanya, ila kwa sasa kitu pekee katika kichwa changu ni kuisaidia Chile katika michezo iliyoko mbele yetu, wawakilishi wangu wanafanya vitu kwa ajili yangu na watakaa na klabu kujua nini ni bora kwa ajili yangu,” alisema Sanchez.

Wakati Chelsea ikiwa inapewa nafasi kubwa ya kumtwaa mwanasoka huyo, tayari kuna habari mpya kwamba timu nyingine zimeonyesha nia ya kumsajili.

Habari zinasema kwamba Sanchez anakaribia kumwaga wino katika klabu ya Manchester City lakini kumejitokeza wapinzani wapya wa man City ambao ni klabu ya Bayern Munich wanaotajwa kumtaka Sanchez kwa nguvu zote.

Upepo umegeuka kwamba Sanchez anaweza kuhamia Munich kutokana na kile ambacho kinatajwa kwamba msukumo mkubwa wa pacha mwenzake katika timu ya taifa ya Chile, Arturo Erasmo Vidal Pardo anayecheza pia katika kikosi cha mabingwa hao wa Ujerumani.

No comments