SANCHEZ NA OZIL ‘WAFUFUA’ MATUMAINI YA KUBAKI ARSENAL


LICHA ya mastaa Alexis Sanchez na Mesut Ozil kuhusishwa na hatua ya kuondoka Arsenal kiangazi hiki, kuna matumaini ya kubaki baada ya kuonekana wamevalia jezi mpya za nyumbani za klabu hiyo katika bango la promosheni ya kuzitangaza jezi hizo zitakazotumika kwa msimu wa 2017/18 ambalo limevuja na kusambaa mitandaoni.

Sanchez na Ozil wote wamebakisha mwaka mmoja katika mikataba yao ya sasa na hawaonekani kuwa na nia ya kusaini tena hali inayowaumiza vichwa mabosi wa Arsenal.

Klabu kubwa kama Manchester City, Bayern Munich na Paris Saint-Germain zinahusishwa na Sanchez aliyekuwa na msimu bora akifunga mabao 30 na ‘kupika’ 13 katika mshindano yote.

Kuna wasiwasi Arsene Wenger akang’ang’ania kubaki na mastaa hao licha ya kuwapo hatari ya kuwatoa bure mwisho wa msimu ujao, na taarifa zinadai kuwa lengo lake kubwa ni kuepusha wasijunge na klabu pinzani katika Premier League.

Inaweza kuonekana wachezaji hao kuvalia jezi mpya za Arsenal kwa msimu ujao ni kutimia kwa lengo la Wenger kuwabakisha, ingawa hii itakuwa si mara ya kwanza mchezaji kuonekana katika jezi mpya ya klabu hiyo, lakini baadaye kuibukia timu nyingine.


Patrick Vieira alishiriki promosheni ya jezi za msimu mpya wa 2005/06, lakini aliishia kujiunga na Juventus na ikawa hivyo pia kwa Robin van Persie msimu wa 2012/13 aliyeibukia kwa mahasimu wao Manchester United.

No comments