SELEMANI MATOLA AANZA "MAMBO" LIPULI FC... alamba mkataba wa mwaka mmoja kuinoa

KOCHA msaidizi wa zamani wa klabu ya Simba, Selemani Matola amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuinoa timu ya Lipuli FC katika msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Lipuli ya mkoani Iringa imefanikiwa kupanda Ligi Kuu msimu huu ikiwa pamoja na Njombe Mji na Singida United.

Akiongea na saluti5, Mratibu wa Lipuli FC, Ayoub Kihwelo alisema wamempa mkataba wa mwaka mmoja kwanza huku wakiendelea kumwangalia na endapo ataonyesha mafanikio zaidi basi watamuongezea kulingana na makubaliano yao.

“Tushaanza kufanya usajili kwa kutumia ripoti ya mwalimu aliyepita, lakini matola nae ana nafasi ya kubadilisha kulingana na kile atakachokiona kimepungua kwenye kikosi kwasababu, yeye ndie kocha mkuu kwa sasa,” alisema.

Alisema, Matola ataanza kuinoa timu hiyo keshokutwa na watakapoanza mazoezi kwenye uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam wataweka kambi ya wiki mbili.


Kihwelo alisema, wanaamini uwezo wa kocha huyo kwa kushirikiana na kamati ya usajili watasajili wachezaji wazuri watakaoiletea timu mafanikio katika Ligi Kuu inayotarajia kuanza agosti, mwaka huu.

No comments