SERENGETI BOYS YAGEUKA "NGORONGORO HEROES"

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema pamoja na kwamba Serengeti Boys wameondolewa kwenye michuano ya Afcon wiki iliyopita, bado wanaendelea na vijana hao na kwa sasa watakuwa wakiwakilisha nchi kama “Ngorongoro Heroes.”

Malinzi amesema kuwa, dira kubwa kwa sasa ni kuhakikisha Tanzania mwaka 2024 inashiriki kwenye hatua za kufuzu kwa ajili ya Kombe la Dunia na kuhakikisha mwaka 2026 inacheza fainali za Kombe la Dunia.

“Nasisitiza kuwa kwamba Tanzania uwezo wa kucheza fainali za Kombe la Dunia tunao,” alisema Malinzi.

“Serengeti Boys kwa kuweza kufanya vizuri, kuweza kutoka sare na Mali, kuwafunga Angola, Misri, Afrika Kusini, Kongo, kutoka sare na Marekani ambazo ni timu kubwa duniani, tumedhihirisha kuwa Tanzania tunaweza, tujiamini na kuhakikisha mwaka 2026 tunacheza fainali za Kombe la Dunia.”

“Hawa Serengeti Boys sasa wamepata jina jipya, wanaitwa “Ngorongoro Heroes”, wamepata udhamini, kwa maana sasa ni kikosi cha taifa cha under 20 ambacho Januari mwakani kitaingia kwenye harakati za kufuzu kucheza fainali za Afrika ambazo bado hatujajua zitafanyika wapi.”

“Lakini pia tunayo Serengeti Boys mpya ambayo ni vijana wetu ambao wako Mwanza na watahamishiwa Dar es Salaam, ni under 15 kwa sasa. Hawa ndio tunatarajia mwaka 2019, Tanzania tukiwa wenyeji wa fainali za Afrika, kwa maandalizi mazuri, ubingwa utabaki hapa nchini,” alisema Malinzi.

No comments