SHIZA KICHUYA "AIREJESHA" JEZI NAMBA 25 KWA EMMANUEL OKWI

UKISIKIA watu walioshiba uungwana ni pamoja na huyu Shiza Ramadhani Kichuya, kiungo mshambuliaji wa wekundu wa Msimbazi, klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

Kichuya anajua kwamba Emmanuel Okwi anakija tena Simba na mojawapo ya masharti makubwa ya Okwi kwa timu zote anazokwenda nje ya Uganda ni kwamba piga ua lazima avae jezi namba 25.

Jezi hiyo kwa sasa inavaliwa na Kichuya ambaye kwa hakika ameitendea haki katika msimu mmoja aliokaa Simba.

Sasa kama ulikuwa unadhani kwamba Kichuya ataing’ang’ania jezi hiyo hata baada ya Okwi kuwasili, utakuwa unafikiri tofauti.

Badala yake Kichuya amekaririwa akisema kwamba yeye hana tatizo atacheza kwa kiwango kikubwa akiwa Simba hata kama atavaa jezi yoyote ile na kwamba Okwi akiwasili tu atachukua jezi yake anayoipenda.

Okwi ni miongoni mwa wachezaji ambao wanatarajiwa kutua katika klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ambapo uongozi wa timu hiyo umekiri kwamba kila kitu kinakwenda vizuri kumrejesha nyota huyo raia wa Uganda.

Mshambuliaji huyo wa Kiganda alipokuwa akiitumikia Simba kwa kipindi chote alikuwa akivaa jezi namba 25 hiyohiyo, lakini hata alipokuwa Yanga na Etoile Du Sahel ya Tunisia pia SonderjysjkE ya Denmark amekuwa akivaa namba hiyo.

Lakini Kichuya amesema kuwa yuko tayari kuachana nayo mara baada ya Okwi kutua iwapo ataihitaji na yeye kuvaa namba yoyote ile atakayopewa.

“Mimi sina shida iwapo Okwi atakuwa Simba na kuitaka jezi yake nitakuwa tayari kuiachia na mimi nivae namba yoyote ile nitakayopewa kwani sina shida, huwa siangalii vitu kama hivyo na ninachokiangalia ni kuona najituma kwa ajili ya timu, hivyo namba yoyote nikipewa ni sawa.”

“Nawakaribisha wachezaji wote wanaosajiliwa lakini kwa sasa ni mapema kusema kuhusu kuwania namba kwa kuwa bado sijawaona, lakini lengo ni kuona naendelea kuwa bora msimu ujao,” alisema Kichuya.


Tayari wadadavuaji wa mambo wameshaanza kuiona safu hatari ya Simba kwamba kama Okwi atawasili akicheza na Kichuya ambao wote wanacheza winga za kulia na kushoto, habari ya Simba itakuwa nyingine kabisa.

No comments