SIMBA KUFYEKA WACHEZAJI KUMI "WAZEMBE" MSIMU UJAO WA LIGI

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili Simba, Zakaria hans Poppe ameanza kazi yake rasmi. Hivi ndivyo unavyoweza kusema.

Kama ilivyo kawaida yake, mwenyekiti huyo ameshawapa taarifa wachezaji wote wa Simba kwamba karibu nyota zaidi ya 10 watafyekwa kwenye usajili wake kutokana na sababu mbalimbali.

Mwenyekiti huyo amesema kwamba kuna wachezaji ambao hawakuwa na mchango wowote katika timu au mchango wao ulikuwa asilimia ndogo sana hivyo hao wajiandae kuondoka Simba.

Amesema klabu ya Simba imepanga kuwabakiza wachezaji 15 pekee kati ya 25 iliyowasajili msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA).

Mwenyekiti huyo amesema kwamba timu hiyo inataka kukiimarisha kikosi chake kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), watakayoshiriki mwakani.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo amesema kwamba bado hawajapokea rasmi ripoti ya kocha wa timu hiyo Mcameroon Joseph Omog lakini tayari Kamati ya Utendaji ilikutana kufanya tathmini ya kikosi chao kwa ajili ya usajili.

Hans Poppe amesema katika kikao hicho wameona wachezaji 10 ambao hawana mchango na kupanga kuwaondoa katika mipango yao ya msimu ujao wa Ligi na michuano ya kimataifa.

Aliongeza kuwa kati ya wachezaji hao kumi, wapo watakaopelekwa kwa mkopo kwa ajili ya kukuza viwango vyao na wengine kuondolewa kabisa.

Amesema katika kuhakikisha msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa wanakuwa bora zaidi, wamepanga kuwaacha wachezaji 10 kati ya hawa 25 ambao Simba ilikuwa nao kwenye msimu wa Ligi uliomalizika.

“Wakati tukiwaacha hao, tumepanga kuongeza idadi ya wachezaji 10, kati yao wanataka wenye uwezo wa kucheza mashindano ya kimataifa, kama unavyojua mwakani tunaiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika hivyo ni lazima tuwe na kikosi imara,” alisema Hans Poppe.

Habari zinasema kwamba mwenyekiti huyo amepania kuwaleta nyota watatu wa kimataifa kutoka nje ya nchi ambao watakuwa na uhakika wa kuiwakilisha Simba katika michuano hiyo na kufika mbali.


Tayari baadhi ya wachezaji wa Simba wameshaanza kuonyesha wasiwasi wa kubaki katika kikosi hicho na mmoja wao amesema kwamba hana uhakika kabisa kuwa katika Simba ijayo.  

No comments