SIMBA SC KUMTAMBULISHA BEKI MNYARWANDA KWA MASHABIKI WAO LEO

SIMBA SC leo inatarajiwa kumtambulisha rasmi kwa mashabiki wake beki mmoja kutoka Rwanda, Munezero Fistion ambaye habari zinasema kwamba tayari ameshawasili jijini Dar es Salaam.

Habari za uhakika zinasema kwamba Munezero anayekipiga Rayon Sport amewasili hapa nchini mwishoni mwa wiki ili kufanya mazungumzo ya kukamilisha taratibu za usajili.

Saluti5 inajua kwamba Simba imemleta beki huyo wa kati kwa ajili ya kuziba nafasi za mabeki wao wawili; Method Mwanjali aliyekuwa anasumbuliwa na majeraha pamoja na Juuko Murshid anayedaiwa kuomba kuondoka.

Taarifa zilizopatikana zimesema kuwa beki huyo wa timu ya taifa ya Rwanda ataonekana kuanzia kwenye michuano ya Sportpesa iliyoanza jana ambapo wekundu hao watacheza dhidi ya Nakuru All Stars.

“Munezero ameshawasili. Tunaweza kumtumia kwenye michuano ya Sportpesa, mashabiki wetu watapata bnafasi ya kumuona hapo,” kilieleza chanzo hicho cha habari.

Pamoja na beki huyo wa Rwanda, Simba imedaiwa kukamilisha usajili wa beki mwingine, raia wa Uganda, Nicholas Wadada ambaye anakipiga katika kikosi cha Vipers FC ya nchini humo.


Wadada ambaye alikuwa kwenye kikosi cha Clanes kilichoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Gabon, nae anatarajiwa kuwasili wakati wowote akiwa na nyota mwingine wa kimataifa wa SC Villa, Emmanuel Okwi ambaye anarejea Msimbazi kwa mara nyingine.

No comments