SIMBA WAMVUTA MSHAMBULIAJI "JEMBE" KUTOKA NIGERIA

SIMBA imeonekana kufanya kufuru nyingine safari hii ambapo imepanda ndege hadi nchini Nigeria na kushusha mtu mmoja matata kabisa.

Baada ya kuona kwamba mmoja wa washambuliaji wake, Ibrahim Ajib amekuwa hana uhakika wa kubaki Msimbazi, matajiri wa klabu hiyo wameamua kumleta katika kikosi hicho mshambuliaji hatari wa klabu ya Enugu Rangers ya Nigeria, Obinna Nwobodo.

Habari ambazo saluti5 zimezipata zinasema kuwa Simba imeamua kuachana na mpango wa kumsajili Kipre Tcheche ambaye anacheza soka nchini Oman kutokana na masharti yake kuwa magumu.

Kipre amedaiwa kutoa masharti kwamba anaomba asajiliwe pamoja na pacha wake Kipre Balou ambaye walikuwa wote katika Azam FC, sharti ambalo limekuwa gumu kwa Simba kutokana na idadi ya viungo ambao ni wazuri katika kikosi hicho.

“Tumeamua kuachana na Kipre ingawa bado tunaweza kumalizana nae, tumeona tuangalie mtu mwingine. Obinna ametuvutia zaidi kwa sababu amewahi kucheza hata Ulaya,” kimesema chanzo chetu.

Fowadi huyo anadaiwa kuwa nae anataka kubadili upepo wa maisha na kuja Tanzania na analetwa kutokana na mapendekezo ya kocha wa Simba, Joseph Omog.

“Kocha anamfahamu kijana huyo na ametuhakikishia kwamba Simba wanaweza kumsajili kwa sababu ni mtu wa kazi na sio fowadi wa kukaa benchi,” amesema.

Kinachowavutia Simba kwa Obinna ni kuwa ni fowadi msumbufu na ana kasi kubwa uwanjani lakini pia bado ni kinda ambaye ndio kwanza ana miaka 20 hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kumtumia.


“Tunatarajia kumpa mkataba wa miaka miwili. Tunajua atakuwa msaada mkubwa sana kwetu. Tulitaka kuwalea zaidi wachezaji wetu wa ndani lakini kama wanaringa tunafanyaje?” kimesema chanzo hicho.

No comments