SIMBA YASEMA NIDHAMU MBOVU NDIO ILIYOMPONZA HAMAD JUMA KUTUPIWA VIRAGO

HIVI karibuni Simba imeachana rasmi na beki wake wa kulia, Hamad Juma ambaye ilimsajili kutoka katika kikosi cha Coastal Union ya Tanga msimu uliopita.

Saluti5 inajua kwamba Hamad ambaye alitarajiwa kucheza kwa kiwango kikubwa katika Simba, ameachwa kutokana na utovu wa nidhamu.

Habari zilizopatikana zinasema kwamba Hamad alianza kuonyesha tabia zake za utovu wa nidhamu mapema tu baada ya kusajiliwa na alionywa mara kadhaa lakini hakubadilika.

“Tumeamua kuachana na Hamad, kuna wakati alikuwa anafanya mambo ambayo Simba tuliona ni kama mtoto wetu na tulimkalisha chini tukidhani kuwa atabadilika lakini hakuonyesha dalili ya kufanya hivyo,” alisema kiongozi mmoja wa Simba.

“Kutokubadilika kwa Hamadi kumeigharimu sana Simba kwani kuna wakati beki mwenzake, Javier Besela Bokungu alikuwa anatumnikia adhabu ya kadi, kocha Omog akalazimika kumpanga kiungo Muzamir Yassin katika nafasi hiyo.”

“Imekuwa bahati mbaya ni kwamba Hamad amekuwa ni mchezaji wa kwanza kuachwa lakini ana umri mdogo akibadilika anaweza kuwa na manufaa huko mbele ya safari lakini sio kwa Simba hii ya sasa ambayo kiwango cha nidhamu kinatakiwa kiwe cha juu sana,” amesema.


“Unajua tulimwacha Malika Ndeule tukampeleka kwa mkopo Majimaji na hapo ndipo unaona kwamba hesabu zetu hazikuwa sahihi kubaki na Hamad ambaye tuliamini uwezo wake na mwili wake vingetusaidia,” amesema.

No comments