TAMBWE ATUA JANGWANI, AWAAMBIA WANA YANGA "TULIENI WANANGU"

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe amewasili jijini Dar es Salaam Jumanne hii tayari kwa kuja kumalizana na uongozi wa timu hiyo, lakini akawaambia Wanayanga watulie.

Akiongea na saluti5, Tambwe amesema baada ya kuwasiliana na mabosi wa Yanga katika mazungumzo ya awali ya kusaini mkataba mpya, amekuja kumalizana nao.

Tambwe amesema kuwa bado anaona Yanga ndio sehemu sahihi kwake ambapo anataka sasa kuhakikisha timu yao inafika mbali katika mashindano ya msimu ujao mbali na Ligi ya mabingwa Afrika.

Mshambuliaji huyo amesema kuwa baada ya mapumziko, sasa mwili wake uko tayari kuanza kazi ya kufunga mabao ambapo alizungumzia usajili unaofanywa na timu hiyo akisema akili kubwa inatumika na kwamba yanga itatisha msimu ujao.

“Nimekuja kumalizana na Yanga, nilikuwa nazungumza na viongozi wakanambia nije ili tumalizane, nawasubiri wajipange ili nisaini mkataba,” alisema Tambwe.

“Usajili nilikuwa naufatilia tangu nikiwa nyumbani Burundi, naona mambo yako vizuri, wachezaji waliosajiliwa ni wazuri na nafikiri hili litatupa sura mpya kwa msimu ujao.”   

No comments