TOT TAARAB, ZANZIBAR STARS KUPIMANA UBAVU MANGO GARDEN IDD PILI

BENDI mbili kongwe za mipasho Bongo; Tanzania One Theatre (TOT) na Zanzibar Stars Modern Taarab  iliyorejea upya hivi karibuni, zinatarajiwa kupimna ubavu siku ya Idd Pili ndani ya Mango Garden, Kinondoni, Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya bendi hizo zinasema kuwa, kwa sasa kila bendi iko kambini ikijiandaa na pambano hilo linalotazamiwa kuwa la kukata na shoka kutokana na bendi zote kuwa na nyimbo kali.

Mbali na kuwa na nyimbo kali, Zanzibar Stars na TOT Taarab zinajivunia pia kwa kuwa na mashabiki kila kona ya jiji la Dar es Salaam na hata mikoani, ambao wanatarajiwa kufika kwa wingi kuzipa bendi zao ‘amsha amsha’ ya kiushindani.

Wakati TOT Taarab ikiringia wasanii wake mahiri kama vile malkia Khadija Kopa, Abdul Misambano, Ally Star na Mwasiti Suleiman, Zanzibar Stars nayo inajiamini kwa mastaa wake wa muda mrefu wakiwemo Zuhura Shaaban, Mwanahawa Ally, Sabah Muchacho na Jokha Kassim.


Kiingilio katika shoo hiyo ya kindumbwendumbwe, kitakuwa ni buku nne tu kwa wale watakaopenya ukumbini kabla ya saa 4:00 usiku na baada ya muda huo, mtonyo wa 6,000 utahusika kwa kila atakayetaka kuingia.

No comments