"UYANGA" WAWAKWAMISHA WACHEZAJI WAWILI KUSAJILIWA SIMBA

WAKATI ambapo klabu ya Simba ikiendelea na usajili wake wa “hatari”, kuna taarifa kuwa wachezaji wawili wamekwama kupata nafasi ya kusajiliwa kutokana na sababu mbalimbali.

Taarifa za siri kutoka ndani ya vyanzo mbalimbali zinabainisha kuwepo kwa majina ya baadhi ya wachezaji wapya walioshindwa kukidhi vigezo vya usajili, huku sababu kubwa ni kukwepa kuchukua wanandinga walio na mahaba ya timu hasimu, Yanga.

Chanzo makini cha habari za usajili wa msimu ujao kimeiambia saluti5 Alhamisi kuwa wachezaji wawili waliongizwa katika rada za kusajiliwa wana damu za “Uyangayanga”, hivyo wameshindwa kukidhi masharti ya kuwemo kundini.

Hata hivyo, taarifa hizi zimeminya majina ya wachezaji kutajwa bayana kutokana na sababu maalum.

Imebainika kuwa awali majina ya wachezaji hao yalikuwa yakitajwa katika orodha ya wanandinga wapya waliokuwa na nafasi kubwa ya kusajiliwa katika kikosi cha msimu ujao ch wekundu wa Msimbazi, lakini walipobainika walikuwa na malengo na kujiunga na wana Jangwani wakafungiwa mlango wa mazungumzo.

“Kamati imekuwa makini sana katika zoezi la usajili linaloendelea, kubwa ni kujiaminisha kama wanaosajiliwa wana moyo wa dhati wa kuitumikia Simba kwa moyo.”


“Vigezo hivi ndivyo vinavyofanya usajili wa msimu huu kuwa makini na hii inatokana na ukweli kuwa baadhi ya wachezaji wa msimu uliopita walishindwa kuitumikia timu kwa mapenzi, hivyo walichangia kuifanya Simba kukosa ubingwa na uwakilishi wa michuano ya kimataifa mwakani,” kilisema chanzo makini cha habari hizi.

No comments