VIONGOIZI WA YANGA WAPANGA KUMVAMIA MANJI OFISINI KWAKE

MKUTANO wa viongozi wa Yanga umeibuka na maazimio magumu ndani ya klabu yao wakipinga kuondoka kwa mwenyekiti wao, Yusuph Manji lakini pia wanataka kufanya maamuzi magumu ya kuvamia ofisi za bilionea huyo.

Mkutano huo ulifanyika juzi makao makuu ya klabu hiyo Jangwani na kuhudhuriwa na makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga, Katibu Mkuu Charles Mkwasa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya Utendaji, viongozi hao waliutaka uongozi wao kutokata tamaa kumshawishi Manji kurudi kwenye uongozi na kwamba hata wao hawakubaliani na maamuzi ya mwenyekiti huyo.

Taarifa zinasema viongozi hao wamemtaka Manji kuhakikisha anarudi kuendelea na kwamba suala la kuumwa kwake hawaoni kama ni sababu mwafaka kwa kuwa yeye si mtendaji wa kila siku wa kazi za Yanga ambapo atakuwa akisaidiwa majukumu mengi na makamu wake na sekretarieti.

Viongozi hao pia wanajipanga kuhakikisha kila tawi linakusanya wanachama wao kisha kumvamia Manji katika ofisi yake kupeleka kilio chao kumtaka arudi upya pia kuutaka uongozi wao kuitisha uongozi wa dharura kumjadili Manji.

“Kuna mambo tumekubaliana kimsingi ambayo tumeutaka uongozi kuyafanyia kazi, kwanza ni kwamba hatukubaliani na maamuzi ya Manji kuondoka, angalia tangu ameondoka hakuna aliyeweza kuziba yale aliyokuwa akiyafanya,” alisema mmoja wa viongozi hao.


“Ukiachana na hilo pia tumejipanga wenyewe, tunataka kumfuata Manji pale ofisini kwake tukiwa na wanachama wetu na hilo litafanyika kutoka kila tawi tukutane kisha tumfuate tumwambie tunamtaka arudi, unajua hata kama anasema anaumwa mbona kazi zake ofisini kwake anafanya, huku Yanga atakuwa akisaidiwa na wasaidizi wake.”

No comments