WANYARWANDA WA DAR ES SALAAM WAMIMINIKA UWANJANI KUMPIGIA DEBE FISTON MUNEZERO SIMBA

BEKI mpya anayewania kusajiliwa na Simba, Fiston Munezero kutoka klabu ya Rayon Sports ya Rwanda alikuwa mmoja wa watu wanaotazamwa na mashabiki wengi uwanjani Jumanne iliyopita.

Simba walimjaribu beki huyo raia wa Rwanda katika mechi dhidi ya Nakuru All Stars kwenye mchezo wa Kombe la Sportpesa na akaonyesha uwezo mkubwa.

Lakini nje ya dimba pia kulikuwa na baadhi ya mashabiki wa Simba raia wa Rwanda ambao walikuwa wakimpigia debe beki huyo, wengine wakiwa wamevaa jezi yake aliyokuwa anachezea katika klabu yake ya zamani.

Fiston alivaa jezi namba 21 katika mechi dhidi ya Nakuru, jezi ambayo huwa inavaliwa na beki mwingine wa kati wa Simba, Novatus Lufunga ambaye hakucheza siku hiyo.

“Jamaa amejipanga sana, hata huko kwao akicheza huwa kuna mashabiki wanaingia na mabango yenye ujumbe wa kumtia presha awasaidie,” amesema shabiki mmoja.

Lakini shabiki aliyevaa jezi ya Fiston ambaye ni raia wa Rwanda amesema kwamba katika kikosi cha Rayon, mchezaji huyo ndie mhimili wa timu nzima.

“Sijui Simba watamsajili au la, lakini kule Rwanda unapomtaja Fiston unakuwa umetaja unakuwa umetaja mmoja wa watu wanaoibeba Rayon. Kama atahamia hapa maana yake Simba itakuwa imebomoa ukuta wa Rayon kwa kiwango kikubwa sana,” amesema.


Walipoulizwa kama wamekuja na beki huyo kama wapambe wa kumsaidia kumpigia debe, mashabiki hao walisema kwamba wao ni Wanyarwanda wanaoishi hapa Tanzania na waliposikia kwamba Fiston anacheza wakaona wavae jezi yake kumpa sapoti afanye vyema uwanjani.

No comments