YANGA SASA YAMNYATIA BEKI KIRAKA WA MBAO FC... si mwingine ni Jamal Mwambeleko

YANGA imeanza usajili wake kwa kasi kubwa na baada ya kufanya mazungumzo na mshambuliaji Mbaraka Yusuph, tayari kikosi cha usajili kimehamia kwa beki wa Mbao FC, Jamal Mwambeleko ambaye atatua wakati wowote wiki hii.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba tayari uongozi wa timu hiyo umeshakutana na Jamal katika kumsajili ambapo karibu kila kitu wameshakubaliana juu ya mambo ya msingi.

Jamal anahitajika Yanga baada ya kumvutia kocha George Lwandamina ambapo anakuja kusaidiana na Haji Mwinyi katika nafasi ya beki wa kushoto, huku Oscar Joshua akitupiwa virago.

Bosi mmoja wa Yanga amesema endapo timu yao itamnasa Mwambeleko itakuwa imeziumiza Simba na Mbeya City zilizokuwa zinamnyatia kinda huyo ambaye pia kocha wake wa zamani wa Mbao FC, Etiene Ndayiragije alimzuia kusajiliwa na timu yoyote bila kumtaarifu.

“Tunamsajili mapema wiki. Huyu Jamali ni beki mzuri sana, utamu zaidi ni kwamba anaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani, jambo ambalo litakuwa ni faida kwa timu yetu,” alisema bosi huyo.


“Tumezungumza nae juzi na kila kitu kinakwenda sawa, hakuna shida upande wetu wala hakuna shida upande wa mchezaji kutokana na kwamba amemaliza mkataba wake na timu yake ya Mbao.”

No comments