YANGA YAKIRI KUPIGWA BAO NA SIMBA SABABU YA UKATA UNAOWAKABILI

YANGA imepokonywa wachezaji watatu mahiri waliosajiliwa na Simba ambao ni mshambuliaji mmoja, kipa na beki, lakini kikwazo ni kukosekana kwa fedha za usajili baada ya kujiondoa kwa mwenyekiti wao, Yusuph Manji.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba klabu hiyo imepokonywa mshambuliaji John Bocco, kipa Aishi Manula na beki wa kushoto wa Mbao FC, Jamal Mwambeleko ambao wamesajiliwa Simba kutokana na kukosekana kwa fedha za usajili.

Bosi mmoja amesema kuwa licha ya Yanga kuingia mkataba na Sportpesa, bado klabu hiyo imeshindwa kupata fedha za kuwezesha kufanyika kwa usajili ambao unakadiriwa kutafuna kiasi cha sh. mil 600 kukamilisha zoezi zima.

Aliongeza bosi huyo akisema jambo hilo lingekuwa rahisi endapo Manji angebaki ndani ya klabu hiyo ambapo ndie alikuwa akimwaga fedha hizo na kuifanya klabu hiyo kuendelea kusota kuingia katika zoezi la usajili kwa kuingia mikataba na wachezaji waliotakiwa.

Awali Yanga ililetewa jina la Bocco aliyetakiwa na kocha wa timu hiyo, George Lwandamina na Manula, lakini kukosekana kwa fedha kukafanya kuwaniwa na Simba kabla ya mwishoni mwa wiki Mwambeleko aliyetangulia kufanya mazungumzo na Yanga, nae kusaini klabu hiyo.

“Tulikuwa tunawataka wachezaji hao wote, kocha alituletea majina yao tukafanya nao mazungumzo, lakini kukosekana kwa fedha ndio tatizo kubwa,” alisema bosi huyo.


“Kuna wajumbe wa Kamati ya usajili, akina Bin Kleb na hata Seif Magari wamekubali kufanya majukumu yao ya usajili lakini wamehoji kuwa bila Manji usajili huo utafanyikaje? Wakashauriana ni lazima juhudi zifanyike kumshawishi Manji arudi.”

No comments