YANGA YAPOTEZEA TETESI ZA DEUS KASEKE KUTIMKIA SINGIDA UNITED MSIMU UJAO

KLABU ya Yanga imesema haifahamu kama kiungo wake, Deus Kaseke ametimka klabuni humo.

Taarifa za ndani kutoka kwenye klabu hiyo zinasema kuwa mchezaji huyo yupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili kwenye klabu ya Singida United iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.

Singida imeanza usajili kwa kasi baada ya kumsajili kocha wa zamani wa Yanga na mkurugenzi wa ufundi, Hans Plijium na wachezaji watano wa kimataifa.

Mbali na hao, Singida imehakikisha inaimarisha vyema kikosi chake baada ya kumsajili kiungo mahiri wa Mbeya City, Kenny Ally.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema bado wanaamini kaseke ataendelea kubaki Yanga kwa ajili ya msimu ujao.

“Tunachofahamu ni kuwa Kaseke bado ni mchezaji wa Yanga na ataendelea kuwa katika mipango ya kocha, tunamuamini Kaseke na tunaamini ataendelea kuitumikia Yanga msimu ujao,” alisema Mwambusi.

Kocha huyo wa zamani wa Mbeya City amesema Kaseke bado yupo kwenye mipango ya kocha George Lwandamina kwa ajili ya msimu ujao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

No comments