ZIDANE: TAARIFA ZA NYOTA WANGU KUHAMA REAL MADRID HAZINIPASUI KICHWA

NI kama maamuzi magumu lakini haina namna kwa kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane ambaye amesema kwamba hana presha hata kidogo anaposikia kuwa kuna wachezaji muhimu wanataka kuondoka.

Kuonyesha kwamba hababaiki, Zidane amesema kuanzia msimu ujao atahakikisha kinda wake, Jesus Vallejo atakuwa ndie mrethi wa kiraka wake wa muda mrefu katika kikosi hicho, Kepler Laveran LimaFerreira maarufu kama “Pepe” ambaye anadaiwa kuondoka katika miamba hao wa soka barani Ulaya.

Amesema kwamba Jesus Vallejo mwenye umri wa miaka 20 anaweza kabisa kuwa chaguo sahihi kwenye nafasi ya ulinzi katika msimu wa Ligi wa mwaka 2017/18 kuchukua nafasi ya Pepe mwenye miaka 34.

Zidane amesema kuwa baada ya kukaa katika klabu hiyo kwa miaka 10, Pepe anaweza kuondoka na kazi ambayo ameifanya akiwa Santiago Bernabeu haina mfano.

Kocha huyo ameliambia Shirika la Habari la Kichina la Xinhua kwamba Pepe anaweza kukumbukwa na kila mmoja katika klabu yake kwa uwezo wake mkubwa.

Hata hivyo amesema kwamba, kutokana na uwezo mkubwa alioonyesha Vallejo ambaye alisajiliwa kutoka klabu ya Real Zaragoza mwaka 2015 hana wasiwasi kwamba nafasi hiyo iko salama.

Mchezaji huyo alikuwa kwa mkopo katika klabu ya Eintracht Frankfurt ya Ujerumani na Zidane anaamini kwamba kutokana na ugumu wa Ligi hiyo, Vallejo sasa atakuwa jiwe gumu kulivunja katika ukuta wa kikosi chake.


“Kila mmoja anajua ugumu wa Ligi ya Ujerumani, mchezaji anapokuwa kule na akapata nafasi ya kucheza zaidi ya mechi 20 katika Ligi hiyo ni mzoefu sana. Vallejo amecheza mechi 25 kule, hapa kwetu ni kama anakuja beki mgumu zaidi,” amesema.

No comments