ZINEDINE ZIDANE "AMWANGUKIA" CRISTIANO RONALDO

KOCHA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amemwangukia straika wake, Cristiano Ronaldo baada ya kumpigia simu akimbembeleza asiondoke katika klabu hiyo kwa kile alichodai bado wanamwitaji sana.

Hatua ya Mfaransa huyo imekuja baada ya mwishoni mwa wiki staa huyo mwenye umri wa miaka 32 kuueleza uongozi wa klabu hiyo kuwa anataka aondoke kutokana na kuandamwa na kashfa ya ukwepaji kodi na huku taarifa zikieleza kuwa ana mpango wa kurejea kwenye klabu yake ya zamani ya Manchester United.

Mazungumzo ambayo yalionekana kupamba vichwa vya vyombo vya habari nchini Hispania yanaripotiwa kuuweka roho juu uongozi wa klabu hiyo, akiwemo kocha huyo ambapo juzi aliamua kumpigia simu ili kumbembeleza.

Msimu uliopita mshindi huyo wa tuzo ya mchezaji bora wa dunia Ballon d’Or mara nne ulikuwa ni wa mafanikio kwa klabu hiyo ya Bernabeu.

Lakini sasa anaonekana kuwa na mawazo kuwa hamlindi vyema baada ya kufunguliwa mashitaka hayo ya kukwepa kodi yenye thamani ya pauni mil 13.

Kutokana na hali hiyo, gazeti la Marca lilidai kuwa Zizou alipiga simu hiyo kwa straika huyo wa timu ya taifa ya Ureno licha ya kuwa alikuwa mbali kwenye mapumziko na familia yake nchini Italia, akimwelezea kuwa bado anahitajika.

“Cris bado tunakuhitaji” gazeti hilo lilikariri sehemu ya mazungumzo baina ya pande zote mbili.


Lilieleza kuwa Zidane anamuona Ronaldo kama bado nguzo muhimu kwenye klabu hiyo licha yakuwa umri unakwenda na inaripotiwa kuwa tayari kumlipia deni hilo la pauni mil 13 ili aweze kuendelea kubaki.

No comments