AJIB: NIMETUA YANGA ILI KUTIMIZA NDOTO YANGU YA KUTWAA MATAJI MFULULIZO

MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Ibrahim Ajib amesema kuwa moja kati ya sababu kubwa zilizomvuta kutua Jangwani, ni pamoja na kutimiza ndoto ya kutwaa mataji mfululizo, jambo alilokuwa akilikosa alipokuwa kwenye klabu ya Simba.

Ajib amesema kuwa akili na mawazo yake kwa sasa vinawaza kuwa sehemu ya mafanikio katika timu yake mpya ya Yanga aliyojiunga nayo hivi karibuni.

“Nadhani kila mchezaji anakuwa na shauku ya kubeba mataji, unapoona sehemu uliopo kuna ugumu wa kufikia ndoto zako ni wazi unapaswa kubadilisha upepo, Yanga ni sehemu salama kwangu, naamini naweza kukata kiu yangu ya kutwaa mataji,” alisema Ajib.

“Nina muda mfupi toka nisaini hapa lakini kuna ushirikiano mzuri kuanzia kwenye benchi la ufundi mpaka kwa wachezaji wenyewe na hiki ndio nilichokuwa nakitaka,” aliongeza Ajib.

Ajib alisema, kwa sapoti hiyo anachokiweza kwa sasa ni kujifua vya kutosha ili aweze kufanya vizuri kwa kuipa timu hiyo mafanikio.

Alisema, anajua Yanga ni timu kubwa na ndio mabingwa wa Ligi, hivyo atajitahidi kushirikiana na wachezaji wenzake ili kupata mafanikio hayo.


Ajibu anatarajia kuanza msimu akiwa na jezi mpya ya Jangwani baada ya kuachana na Simba aliyoichezea kwa misimu mitatu tangu apandishwe kutoka kikosi cha vijana.

No comments