ALEXIS SANCHEZ ATAKIWA KUISAHAU MANCHESTER CITY


ARSENE WENGER amekanusha taarifa kwamba Alexis Sanchez alimfahamisha kuwa anataka kuondoka Arsenal na akasisitiza kuwa hatamuuza straika huyo wa kimataifa wa Chile kwa Manchester City.

Wiki iliyopita, ripoti nchini Chile zilidai kwamba Sanchez amemjulisha Wenger nia yake ya kutaka kujiunga na kikosi cha Pep Guardiola kiangazi hiki.

Straika huyo wa miaka 28, ambaye amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake na Arsenal, pia ameelezwa kuzungumza na kocha huyo wa Manchester City kuhusu kuhamia Etihad.

Lakini alipoulizwa Wenger kama Sanchez alimweleza kuwa anataka kuondoka, alijibu “Hapana” na kuongeza kuwa njia rahisi ya kusimamia wachezaji katika mwaka wa mwisho wa mikataba yao ni kuwapa nafasi ya kufanya kadiri ya matakwa yao.

'Hakuna mtu anayejua leo kama Sanchez atakuwa katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake msimu ujao kwa sababu anaweza kuongeza mkataba na sisi mwanzoni mwa msimu au wakati wa msimu,” alisema.

Alipoulizwa kama bado ana nia ya kuendelea kumbakisha straika huyo, alijibu: “Ndiyo, huo ni mwendelezo wa kile nilichosema mwishoni mwa msimu... Hivyo ndivyo tutafanya. Anaongeza thamani kubwa katika kikosi na nadhani pia ni mpenzi mkubwa wa klabu.”

No comments