ASHA BARAKA ASEMA KWENYE MSAFARA WA MAMBA, KENGE NAO WAMO …asema wasaliti hawatavuliwa Twanga PepetaMkurugenzi wa bendi ya The African Stars “Twanga Pepeta”, Asha Baraka amesema wasanii wa bendi yake walioshiriki onyesho la jana Friends Corner Manzese, wanalo wanalolitafuta.

Akiongea na Saluti5 kwa njia ya simu leo mchana akiwa safarini kuelekea Kigoma, Asha Baraka amesema kuwa katika wasanii hao wako waliokubuhu kwa uhujumu wa bendi na wako wanaofuata mkumbo.

“Kwenye msafara wa mamba, kenge nao wamo,” alisema Asha Baraka.

Mkurugenzi huyo wa Twanga Pepeta amesema, kwa sasa yupo safarini na hawezi kuongea lolote hadi atakaporejea na kukaa na uongozi wa bendi kabla ya kuchukua hatua stahiki.

“Kwa vyovyote vile ni lazima tuchukue hatua, lakini kwa sasa siwezi kusema lolote zaidi ya kusema kuwa kila jambo lina mwisho wake, kama hata binadamu anazaliwa na kufa, basi hata usaliti pia una mwisho wake,” alieleza kwa uchungu Asha Baraka.

Asha Baraka akafafanua zaidi juu ya usaliti huo wa wasanii wake: “Onyesho la kwanza wiki iliyopita lilifanyika kienyeji, matangazo yakaanza bila mimi kujulishwa chochote, yaani mimi mwenye bendi nakutana na vipeperushi vinavyohusisha bendi yangu bila idhini yangu wala ya meneja. Kwa shingo upande sana nikakubali wasanii wangu wakashiriki."

“Baada ya onyesho hilo akanifuata Thabit Abdul na kutaka kufanya onyesho lingine Jumanne inayokuja (jana) la bendi yake ya Wakali Wao na Twanga kwa vile kuna pesa wanawadai wanamuziki wa Twanga Pepeta kufuatia makubaliano yao ya onyesho la kwanza.

“Nilimkatalia na kumwambia achague Jumamosi yoyote akafanye show Mango Garden, Kinondoni kwa ajili ya kumalizia vimeo vyao. Nikawaambia pia kama wanataka kufanya onyesho la Jumanne basi iwe kila Jumanne ya mwisho wa mwezi na sio kila wiki."

“Lakini yeye na wasanii wangu bado wakakiuka maagizo yangu na kuitumia Twanga Pepeta kinyemela kwa madai ya kuwa hawajatumia jina bendi. Hii haikubaliki."

“Tuliamua kuachana na show za Jumanne ili wasanii wapumzike na kupata wasaa wa kutengeneza tungo mpya, huwezi kuwa na wasanii wanaofanya kazi Jumanne hadi Jumapili, hakutakuwa na ufanisi.

“Wanasema wanafanya show Jumanne kwa aliji ya kuondoa njaa, hivi njaa inaondoka kwa show moja ya kugawana elfu ishirini ishiri?”

Asha Baraka amesema anawapongeza wale ambao hawakushiriki onyesho hilo na anawasikitikia wale wasanii fuata mkumbo ambao hawajui kuwa kila mmoja aliingia Twanga kwa staili yake na kwa makubaliano tofauti.

“Nimesoma kwamba wametangaza wataendelea kufanya hivyo kila Jumanne, nawatakia kila la kheri lakini nawataka wajue kuwa kwangu mimi kuanza moja huwa si tatizo. Hatutakuwa na muda wa kuvumiliana wala kubembelezana,” aliongeza Asha Baraka.

No comments