AUDIO: JIFAIDIE MOJA KATI YA TUNGO NNE PEKEE ZA RASHID PEMBE VIJANA JAZZ BANDWAPO baadhi ya wanaume ambao mke anapokosea nyumbani hawakosoi papohapo na badala yake wanakwenda kudhihaki pembeni aidha wakiwa na marafiki zao au hata kwa ndugu wa upande wao.

Vijana Jazz “Air Pambamoto” waliliona hili hata mwaka 1989 wakaamua kulianika bayana kupitia kibao “Siri ya Ndani” ambacho ni kati ya vinne  vikali vya aliyekuwa mpulizaji hatari wa domo la bata ndani ya bendi hiyo, Rashid Pembe, vingine vikiwa ni “Baba Sammy”, “Dar es Salaam” na “Mwanamke Salo”.

“Siri ya Ndani” ambacho ni kitu cha dakika 7.30, kimewashirikisha Shaaban Wanted (solo), Agrey Ndumbalo (rythym) na Beka Semhando (bass). Pembe na Said Mohammed "Ndula" walisimama kwenye saxophone na mapafu ya Kulwa Milonge, Hassan Chondoma na Hamis Mnyupe ndio yaliyotumika kwenye tarumbeta.


Tumba katika wimbo huu unaopatikana kwenye albamu ya “Mawifi” ambayo ni ya mwisho kwa marehemu Hemed Maneti, zimepigwa na Haruna Lwali "Tanzania One", drums Juma Choka na kwenye uimbaji walisimama Mohammed Shaweji, Mohammed Gotagota, Abdallah Mgonahazeru, Said Hamis na Fred Benjamin.

No comments