AYA 15 ZA SAID MDOE: MWESABU MAKOSA MAPENZI HAYAJUI, ASANTE CHAZ BABA


“Amerudi Analia” kwangu mimi (nasisitiza kwangu mimi binafsi), ndiyo kazi bora ya mwisho kuisikiliza katika tungo za bendi za dansi.

Wimbo huo wenye zaidi ya mwaka mmoja, utunzi wake Christian Bella, ni kazi kutoka kwao Malaika Music Band.

Sisemi kuwa nyimbo nyingine za bendi zilizotoka baada ya “Amerudi” ni mbaya, la hasha, zipo nyingi nzuri zilizojitahidi kujikongoja, lakini kwa mtazamo wangu naona hazikufikia hatua ya kuitwa nyimbo pendwa - wimbo uliokubalika, wimbo wa taifa (hit song).

“Amerudi” inapoanza tu kupigwa ukumbini shangwe kubwa huibuka, mashabiki hukimbilia kwenye ‘dancing floor' mithili ya watu wanaogombania daladala kwenye uhaba wa usafiri. Sisemi namna ulivyotawala mitaani kuanzia katika vibanda umiza kwa kurekodi nyimbo hadi kwenye maboda boda na bajaji.

Watu ukumbini hucheza wimbo huo kwa hisia kali, wakiuimba huku mikono yao ikiashiria kwa vitendo kile wanachokiimba. Ama kwa hakika huu ni wimbo uliotengenezwa kwa ajili ya kuwashika mashabiki na si kwa ajili ya kumburudisha mwimbaji.

Naam ziko nyimbo ambazo ukizisikiliza tu utajua wazi kuwa huu wimbo ni kwa ajili ya kuishika jamiii na zipo ambazo ukizisikiliza utabaini kuwa zimeandaliwa (aidha kwa bahati mbaya au kwa makusudi) kwa ajili kumridhisha mwanamuziki au wanamuziki, wanajiimbia wao wenyewe na familia zao.

“Amerudi” ndio wimbo pekee wa dansi hapa Tanzania ulioweza kutinga kwenye chati za nyimbo bora (top ten, top twenty nk), za vituo vikubwa vya radio zinapombwa zaidi na ngoma kali za bongo fleva.

Majuzi alinitembelea mwimbaji Chaz Baba, tukapata wasaaa wa kuongea kwa muda mrefu sana sambamba na kunisikilizisha nyimbo zake nyingi mpya ambazo ameshazirekodi studio. Jamaa ana hazina kubwa sana ya nyimbo mpya zinazokidhi soko la sasa.

Moja ya kazi yake niliyoilewa sana ni ngoma aliyoipa jina la “Mwesabu Makosa Mapenzi Hayajui”. Nimeikubali kwa kila kitu kuanzia jina la wimbo, ujumbe ulioko ndani yake, staili ya uimbaji hadi mirindimo ya wimbo.

Kubwa zaidi ni namna wimbo ulivyoonyooka kwenye ujumbe na jinsi ambavyo shabiki anaweza kuukariri kirahisi, hiyo ndiyo moja ya silaha kubwa ya wimbo “Amerudi”.

Nilishawahi kusema kuwa wapo waimbaji na watunzi wanataka kutengeneza nyimbo ngumu mithili ya sahihi za benki - yaani wanadhamiria kabisa mwimbaji mwingine au shabiki asiweze kuuimba au kuunakili kirahisi. Akili za matope hizi.

Natamani wimbo “Mwesabu Makosa Mapenzi Hayajui” wa Chaz Baba ungenyanyuliwa kama ulivyo na kwenda kuimbwa na bendi ya dansi, hakika ingekuwa moja ya silaha kali za kuipandisha juu bendi husika.

Bendi zetu zimekumbwa na ukame wa tungo kali, tungo zenye kutekenya hisia za shabiki, tungo zenye hadithi nyepesi lakini iliyonyooka na kujitosheleza na badala yake zimebakia kutengeneza nyimbo zenye lundo la waimbaji huku kila mwimbaji akija na mada tofauti, mwisho wa siku ndani ya wimbo mmoja kunakuwa na visa vilivyostahili kutengeneza nyimbo nne. Nyimbo inakosa mashiko, haieleweki.

Kwa sasa Chaz Baba ni msanii huru asiye na bendi yoyote, kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu amekuwa hana bendi tangu aachane kiutata na Mashujaa Band, lakini amejua kuutumia vizuri muda wake huo kwa kutengeneza hazina kubwa ya nyimbo mpya ambazo zitakuwa na faida kubwa kwake na kwa bendi itakayomsajili.

Chaz Baba vunja ukimya mdogo wangu, peleka hiyo nyimbo hewani iwe ni ya kwako binafsi kama msanii wa kujitegemea au hata kwa kupitia bendi flani – ikiwa Mashujaa Band au Twanga Pepeta itanoga sana.


No comments