AYA 15 ZA SAID MDOE: TANZANIA BAND FESTIVAL ‘IMEFIA’ WODI YA WAZAZI?


TAMASHA la bendi za Tanzania lililofanyika Leaders Club Jumamosi ya Julai 30, mwaka jana, ilikuwa ni habari njema kwa wapenzi wa muziki wa dansi, tukahisi ndo mwarobaini na nuru ya kuukwamua muziki.

Ama kwa hakika lilikuwa tamasha bab kubwa licha ya mwitikio hafifu wa mashabiki, lakini bendi kibao zilizoshiriki zikiwemo Msondo, Sikinde, Twanga Pepeta, FM Academia, TOT, Mapacha Watatu na nyingine nyingi, zilileta raha isiyo na kifani.

Tukaambiwa tamasha lile lingekwenda hadi mikoani, lakini haikuwa hivyo, hadithi ikaishia Dar es Salaam hiyohiyo Julai 30, 2016 tu.

Hakuna mji wowote mwingine ulioonja au hata kunusa uhondo wa kitu kile adimu. Tukaambiwa tamasha lile lingekuwa endelevu, lingefanyika kila mwaka, lakini leo tukiwa tunalekea kutimiza mwaka kamili tangu Tanzania Band Festival ifanyike, hakuna fukuto, tetesi wala gumzo la uwepo wa tukio hilo la mwaka.

Taratibu ile njozi ya kudhani Tanzania Band Festival ni mwarobaini wa muziki wa dansi inaanza kuyeyuka na hapo ndo unazidi kujiuliza muziki wa dansi umelogwa na nani?

Tanzania Band Festival imekuwa kama mtoto mchanga aliyezaliwa na kuleta furaha kwa wazazi lakini baadae mtoto yule akafariki kabla hata hajatoka wodini – furaha ikageuka huzuni.

Lakini katika hili wala hata sithubutu kuwalaumu waandaaji maana hawakuja kufanya maoyesho ya hisani au kushiriki matembezi ya mshikamano, walikuja kufanya biashara kupitia muziki wa dansi na mwisho wa siku ni lazima waangalie mrejesho wa kile walichopanda.

Tamasha halikuwa na mwitikio mkubwa wa mahudhurio, halikuwa na mwitikio mzuri wa wadhamini, hali inayodhihirisha kuwa mzigo wote wa gharama za tamasha ulibebwa na mwaandaji.

Kama hakuna faida iliyopatikana basi si rahisi kwa mwaandaaji kurejea tena mwaka unaofuata, labda tu kama atakuwa na wadhamini wa uhakika.


Tamasha kama lile lilipaswa kuwaamsha wadhamini waliobobea katika kuwekeza nguvu nyingi kwenye muziki wa kizazi kipya ambao hutawaliwa zaidi na mfumo wa kutumia CD (Playback).

Muziki wa bendi (live) hususan ule wa dansi, ndiyo muziki wa ukweli, muziki ghali, muziki unaotoa ajira kubwa, hivyo anapotokea mwandaaji kama Q Plus umma wa wapenda dansi unastahili kushukuru na kumuunga mkono, hasa kutokana na ukweli kuwa ‘wawekezaji’ (mapromota) wengi hawaamini katika kuwekeza kwenye muziki wa dansi.

Kwanini muziki wa dansi umepoteza mvuto wa biashara? Kwanini muziki wa dansi umebakia kuwa kama kazi ya wito? Lazima kuna hitilafu sehemu, kuna hitilafu kwenye tungo za dansi japo watu hawataki kukubali, lakini tujiulize kwanini tungo za dansi sio kivutio kwa watoto na vijana?

Kuna hitilafu kwenye utawala wa muziki kuanzia ngazi ya bendi hadi kwenye chama cha muziki wa dansi. Kijana mdogo anaposhuhudia rambirambi ya shilingi laki moja inatolewa na taasisi kubwa ya muziki kwaajili ya kifo cha mwanamuziki ‘supastaa’, unategemea ataupenda muziki wa dansi?

Kuna hitilafu kwenye umri wa wanamuziki wa dansi japo watu hawataki kukubali, lakini ukitazama nyuma na kuangalia kwa makini historia za wasanii wa dansi utagundua waling’ara na kupendwa zaidi pale walipokuwa vijana wabichi.

Wasanii wanazeeka na kufariki lakini warithi wao ni wa kuwatafuta kwa tochi, kila mmoja anakimbilia katika muziki wa kizazi kipya, tunabaki kuendelea kuwategemea wanamuziki wa dansi wenye zaidi ya miaka 35, huku wengi wao wakiwa hawana mafanikio makubwa yaliyotokana na kazi ya muziki yanayoweza kuhamasisha vijana wadogo kulipenda dansi.

Katika hali kama hiyo unategemea vipi wapatikane waandaaji wa matamasha ya dansi? Hawajipendi? Wana pesa za kuchezea?

Wacha tuendelee kushuhudia matamasha mengi ya dansi yakifia wodi ya wazazi.


No comments