BARCELONA YAKANUSHA TETESI ZA NEYMAR KUDAIWA KUTOKUWA NA FURAHA KIKOSINI

KLABU ya Barcelona imekanusha vikali taarifa za kwamba, straika wao, Neymar hana furaha ndani ya kikosi hicho, hivyo ana mpango wa kuondoka.

Kutokana na taarifa hizo zimeibuka tetesi kuwa nyota huyo raia wa Brazil ana mpango wa kutua ama kwenye Ligi ya Premier au kutimkia katika mikikimikiki ya Bundesliga.

Hii inatokana na tukio lake la kutaka kuzipiga na Nelson Semedo katika uwanja wa mazoezi na hatua hii inakoleza tetesi la kama shinikizo la kutaka kuondoka na kuhusishwa kutaka kutua katika klabu ya PSG waliotangaza dau nono.

Tayari klabu ya PSG, Manchester City, Bayern Munich na Chelsea zinatajwa katika mbio za kumnasa straika huyo kwa dau linaloelezwa kuvunja rekodi.

Lakini, taarifa za ndani ya Barca zinasema kuwa, klabu hiyo imemweka Mbrazil huyo katika orodha ya wachezaji waliona mkataba wa miaka mingi hivyo haweza kuuzwa ama kwenda katika timu yoyote.

Rais klabu ya Barcelona, Josep Maria Bartomeu ameviambia vyombo vya habari kwamba taarifa hizo ni zakupuuzwa kwasababu Neymar ana mkataba wa milele na klabu yao.

Bartomue amethibitisha kuwa, Neymar tayari ameongeza mkataba mrefu na mazungumzo binafsi baina yao ni kwamba nyota huyo atasalia Barca kwa kipindi kirefu, licha ya tukio lake la hivi karibuni kutaka kuzipiga na mwanandinga mwenzake.

“Neymar ana miaka yote anayotaka kuwa nayo na Barcelona. Ni kati ya wachezaji bora zaidi katika historia ya klabu ya Barcelona,” alisema Bartomue .

“Tuna furaha sana kwa klabu, ni muhimu sana kwa mashabiki, ni muhimu sana kwa mpira wenyewe.”

“Ukomo utaamuliwa na yeye, kwa sasa ana kipaji na malengo makubwa, yapo katika umbo zuri kuendelea kung’aa kwa miaka mingi ijayo,” Bartomue ameviambia vyombo vya habari vya nchini Hispania.

No comments