BAYERN MUNICH YAAMUA KUACHANA RASMI NA MPANGO WA KUMSAJILI ALEXIS SANCHEZ

HII ni kama taarifa rasmi kwamba klabu ya Bayern Munich haina tena mpango wa kumsajili nyota wa Chille anayetaka kuachana na Arsenal, Alexis Sanchez.

Rais wa klabu hiyo Uli Hoeness amesema kwamba kwa sasa hakuna uwezekano tena wa kumsajili nyota huyo kwa sababu ambazo ziko nje ya uwezo wao.

Rais huyo wa Bayern Munich licha ya kutofafanua kwa kina kuhusiana na sababu maalum lakini amedokeza kwamba mchezaji huyo wa Arsenal anataka mshahara ambao haulipiki.

Sanchez mwenye umri wa miaka 28, anatajwa kwamba yuko katika hatua za mwisho kuondoka Emirates msimu huu huku akitajwa kwamba mahali anakokwenda ni katika klabu ya Manchester City kwa thamani ya pauni mil 50.

Lakini habari nyingine zinasema kwamba washauri wa mambo ya michezo wamemshauri Sanchez kufanya jitihada za kuondoka katika kikosi cha Arsenal na uongozi wa klabu hiyo umeridhia.

Kocha Arsene Wenger ameyakubali mambo yanayotokea sasa na amesema kwamba hana wasiwasi kwamba nafasi ya Sanchez itazibika kirahisi.

Klabu hiyo imekuwa ikihusishwa na kumsajili mshambuliaji hatari wa Monaco anayewindwa na PSG, Kylian Mbappe lakini pia akimuwinda nyota mwingine mwenye jina kubwa duniani, Lacazette.

Kocha wa Bayern, Carlo Ancelotti akizungumzia suala la nyota huyo raia wa Chile amesema kwamba Sanchez ni mchezaji mzuri lakini mwenyekiti wa klabu hiyo Karl Heinz Rummenigge ameshitushwa na mshahara ambao nyota huyo anautaka.


“Sijawahi kusema kwamba Sanchez ni mchezaji mbaya lakini kwa vyovyote vile mwenyekiti wangu anajua mpira ni biashara kama unafanya biasha ambayo inakutia hasara ni hatari,” amesema bila kutaja kiwango ambacho Sanchez anataka kulipwa.

No comments