DONALD NGOMA: LAZIMA NIFANYE KITU KUILIPA FADHILA YANGA YANGU

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Yanga, Donald Ngoma raia wa Zimbabwe amesema kuwa anahisi ana deni ndani ya moyo wake ambalo anapaswa kulilipa baada ya kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu bara na ile ya Klabu Bingwa Afrika ambayo watashiriki.

Ngoma amesema kuwa viongozi wa klabu ya Yanga wamekuwa waungwana kwake katika kipindi chote ambacho alikuwa nje ya kikosi akiuguza majeraha ya goti na kuhusishwa kutaka kutua kwenye kikosi cha Simba.

“Nipo fiti kimchezo baada ya kupona kabisa jeraha langu la goti, nadhani ni muda wangu wa kulipa fadhila kwa viongozi baada ya kunivumilia kwa kipindi kirefu,” alisema Ngoma.

“Yanga ni sehemu tofauti kabisa kwa sababu pamoja na kukaa nje ya kikosi kwa muda mrefu lakini nimepokelewa kwa mikono yote miwili sambamba na kupewa mkataba, klabu imeonyesha nia ya kuendelea na mimi katika mazingira yote hivyo napaswa kulipa fadhila Ligi zitakapoanza,” aliongeza Ngoma.


Ngoma hivi karibuni amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga, timu ambayo ameitumikia kwa mafanikio makubwa akitokea FC Platinumz ya nchini kwao Zimbabwe.

No comments