EVERTON YATHIBITISHA MAJERUHI ROSS BARKLEY ATAKUWA NJE KWA WIKI KADHAA

KLABU ya Everton imekiri taarifa za kwamba Ross Barkley kwa sasa ni majeruhi na atakuwa nje kwa majuma kadhaa, hivyo hatakuwepo katika mechi za mwanzoni mwa msimu huu.

Msimu wa Ligi Kuu England unatarajiwa kuanza katikati ya mwezi Agosti na kiungo huyo amethibitika kuwa atalazimika kuwa nje ya dimba kwa majuma manne.

Tovuti ya klabu ya Everton imeripoti taarifa ya kwamba kiungo huyo amefanyiwa upasuaji wa sehemu ya kifundo cha mguu, hivyo anahitaji mapumziko ya mwezi mzima.

Kutokana na upasuaji huyo, Barkley mwenye umri wa miaka 23 ameshindwa kuambatana na timu katika ziara ya mechi za kujipima uwezo na kabla ya kuanza kwa Ligi zilizofanywa katika nchi za Tanzania na Netherlands.

“Upasuaji ulifanyika vyema na unaendelea kupona vizuri na anatarajia kuanza mazoezi mwishoni mwa juma la tatu kabla ya kuwa fiti kuwemo kikosini,” ilieleza sehemu ya taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa Jumatano iliyopita.

Barkley ambaye ni tegemeo la kikosi cha Goodison, hata hivyo bado hajaketi na uongozi kwa ajili ya kuamua mustakabali wa kandarasi yake iliyofikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.


Everton wanatarajia kuanza Ligi kwa mchezo wao wa kwanza kwa kuumana na Stoke City, mechi itakayopigwa Jumamosi Agosti 12, mwaka huu.

No comments