FRED FELIX MINZIRO ATAMANI KUREJEA YANGA SC

KAMA ni mapenzi ya timu basi haya ya Fred Ferix Minziro yamezidi! Kocha huyo amedhihirisha hilo baada ya kukiri kuwa yuko tayari kurejea tena Jangwani wakati wowote kuanzia sasa pindi uongozi utakapohitaji huduma yake.

Hadi hivi sasa Minziro bado hajajua hatma yake ndani ya kikosi cha Singida United alikokuwa akifanya kazi kama kocha msaidizi, lakini amesisitiza kuwa iwapo Yanga watamwekea mzigo mezani basi yuko tayari kutua kikosini hapo.

Kocha huyo aliyeipandisha Singida na nafasi yake kuchukuliwa na Hans van Pliujim na yeye kuwa msaidizi, bado uongozi wa timu hiyo unasuasua kumuongezea mkataba.  

Akiongea na saluti5, Minziro alisema kama Yanga wataonyesha nia ya dhati yuko tayari kujiunga na kikosi hicho kinachonolewa na George Lwandamina kuchukua mikoba ya Juma Mwambusi.

Alisema anajiamini na kazi anayoifanya hivyo ametoa muda akiwasikilizia Singida na kama wataendelea kumpotezea atatua kwenye timu nyingine zilizoonyesha nia ya kumuhitaji.

“Mimi ni kocha bwana na kazi yangu ni kufundisha. Kuna ofa nimezipata nawasikilizia Singida tu wiki hii, nikiona bado hawakubaliani na matakwa niliyowapa nitaondoka,” alisema.


Timu zilizoonyesha nia ya kumuhitaji Minziro ni Majimaji, KMC ya Kinondoni na Tanzania Prisons.

No comments