GIGGS ASEMA IWAPO ROONEY ATAPUNGUZA MAJUKUMU BASI ATABAKI OLD TRAFFORD MSIMU UJAO

KOCHA wa zamani msaidizi wa Manchester United, Ryan Giggs amesema kwamba ana uhakika nyota mwenzake wa zamani katika klabu hiyo, Wayne Rooney anaweza asiondoke msimu ujao endapo atakubali kupunguza majukumu.

Kauli ya mkongwe huyo imekuja licha ya nahodha wa timu hiyo kuwa mfungaji bora wa muda wote, lakini hali ya hatma ya staa huyo mpaka sasa haifahamiki kutokana na msimu uliopita kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, jambo ambalo limezua pia tetesi za kwamba anaweza kuitema klabu hiyo ya Old Trafford.

Msimu uliopita Rooney aliweza kucheza kikosi cha kwanza katika michezo 15 ya Ligi Kuu na huku akifanikiwa kupachika mabao matano tu, jambo ambalo pia linamuhusisha kuwa huenda akarejea kwenye klabu yake ya zamani ya Everton ama nchini China.

Hata hivyo, Giggs anasema kuwa anavyoamini staa huyo ataendelea kuitumikia klabu hiyo ya jiji la Manchester.

“Wayne ameshakuwa mfungaji bora apewe nafasi aendelee kufunga mabao,” alisema Giggs. 

No comments