GUARDIOLA ASEMA HAONI NJIA YA MKATO KATIKA KUIWEZESHA MAN CITY KUPATA MAFANIKIO

KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema kwamba anajua kwamba ana jukumu kubwa katika kikosi chake lakini haoni njia ya mkato kupata mafanikio.

Pep amesema kwamba watu wanalalamika kwamba kwanini timu hiyo haijachukua ubingwa lakini hawaoni kama kuna sababu ya kujenga timu baada ya kuondokewa na nyota na sasa anajenga kikosi upya.

Amesema katika hali ya sasa inaweza kuichukua timu hiyo miaka 10 kusimama imara na kuwa moja ya klabu tishio zaidi barani Ulaya kama zilivyo timu nyingine kubwa barani humo.

Guardiola alishindwa kufika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kung’olewa na Monaco hii ikiwa ni mara ya kwanza katika histori yake ya kufundisha timu maarufu barani humo.

Lakini Guardiola amesema kwamba kuna wakati mashabiki hawataki kuwa wavumilivu na amesema kwamba hali ikiwa hivyo huwa inamchukua kocha kuyasaka mafanikio kipindi kirefu.

“Mwaka huu hatukuwa kwenye nafasi nzuri lakini kila mmoja anafahamu kuwa hata Barcelona haikuwahi kufika nusu fainali kila mara. Huo ndio mpira ulivyo, kuna wakati haya lazima yatokee,”amesema katika mahojiano na gazeti la L’Esportiu.

“Man City ni klabu kubwa, imecheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya kwa miaka mitano, sasa ni klabu pekee katika Ligi ya Uingereza kufanya hivyo.

Lakini kuyafikia mafanikio ya Barca, Madrid, Munich, Juventus hiyo ni kazi nyingine inaweza kutuchukua miaka 10,” amesema.

Guardiola tayari katika kuimarisha kikosi chake amewasajili Bernardo Silva na kipa Ederson Moraes pamoja na mkulugenzi wa michezo, Txiki Begiristain huku wakikaribia kufunga pingu za maisha na Dani Alves, Benjamin Mendy na Kyle Walker.


“Kwa sasa tukiwa na Txiki tunajaribu kusuka kikosi ambacho tuna uhakika kabisa kitakuwa cha hadhi kubwa katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ingawaje kama nilivyosema si lazima tuwe sawa na hizi timu kubwa zaidi,” amesema Guardiola.

No comments