HAJI MANARA AWATOA WASIWASI WANASIMBA KUHUSU USAJILI

SIMBA imesema kwamba haina haja ya kuwa na wasiwasi wa muda wa dirisha la usajili kufungwa kwa sababu usajili wao ni wa viwango na kasi.

Afisa wa habari na mawasiliano wa klabu hiyo Hajji Manara amesema kwamba klabu yake haina wasiwasi kwasababu siku zote iko makini katika mambo ya usajili.

Manara alikuwa anaulizwa kuhusu tishio la shirikisho la soka Tanzania (TFF) na bodi ya Ligi,vyombo ambavyo vimesema kwamba hakutakuwa na muda wa nyongeza kwa klabu ambayo itashindwa kusajili wachezaji wake kwenye mfumo wa usajili TMS.

“Simba hatuna wasiwasi wowote, sisi siku zote tuko makini na mwaka huu usajili wetu ni wa kiwango na kasi, hatuna mashaka yoyote,” amesema Manara wakati akihojiwa jijini Dar es Salaam.

Amesema kwamba mashabiki wa Simba hawana haja ya kuwa na wasiwasi pia kwasababu Simba imesajili wachezaji wa uhakika na kwamba usajili wa wachezaji wengine ama watatu hivi unakamilishwa.

“Kuna hao ambao tumeshawatambulisha, lakini kuna wachezaji wengine majina yao tutayatangaza hivi karibuni,” amesema Manara.

Manara amewataja baadhi ya wachezaji wa Simba waliosajiliwa, lakini hakutaja baadhi ya majina ambayo yamekuwa yakitajwa kwenye magazeti na mitandao ya kijamii.

Alipoulizwa kwa nini hataki kuwataja wachezaji hao wanaokusudiwa kusajiliwa na Simba, amesema kwamba Simba haiwezi kuingia kwenye mtego wowote kwa sasa.

“Sisi tuko makini, hatuwezi kuingia kwenye mtego huo,” amesema Manara.

No comments