HAMIS KIIZA ATAMANI KUREJEA TENA SIMBA SC

STRAIKA raia wa Uganda, Hamis Kiiza ambaye aliondoka katika kikosi cha Simba baada ya kudaiwa kukosa nidhamu, amesema kwamba anatamani kurejea Simba.

Kiiza ameyasema hayo katika mahojiano kutoka nchini Sudan anakochezea soka katika klabu ya Al Hilal Elobeid FC ambayo imekumbana na rungu la Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Katika mahojiano hayo, Kiiza amesema kwamba anawashikuru sana watanzania kwani wamekuwa wakimuunga mkono siku zote na kuna siku moja anaweza kurejea Tanzania.

“Kuna siku naweza kurejea Tanzania kwani nimeishi huko kwa wema sana katika timu zote, kuna siku nitarejea,” amesema Kiiza ambaye aliondoka Simba akiwa mfungaji bora wa msimu katika kikosi hicho.

Shirikisho la Soka Duniani limeibana Sudan kwa kuifungia baada ya serikali ya nchi hiyo kuingilia mambo ya mpira wa miguu nchini humo.

Awali kulikuwa na habari kwamba mshambuliaji mwingine wa Uganda, ambaye ametua Simba kwa mara nyingine, Emmanuel Okwi, amekuwa akiwaomba viongozi wa Simba kumrejesha ili wamshirikishe nae katika kikosi hicho.


Okwi anaamini kwamba pamoja na mapungufu yake ya kinidhamu, lakini wakisimama katika eneo la hatari, mabeki wa timu nyingine watalazimika kutafuta namna ya kuwalinda.

No comments