HANS POPPE, MO DEWJI WAKAMATA USUKANI MWENDELEZO WA USAJILI SIMBA

SIMBA wapo kamili gado! ndivyo ambavyo ukiulizwa na mtu yeyote unaweza kusema.

Hawana wasiwasi wametulia na wanaendelea na mipango yao ya kusuka kikosi cha ushindi kwa ajili ya Ligi Kuu msimu ujao na michuano ya kimataifa.

Baada ya viongozi wake wakuu rais Evan Eveva na makamu wake Geofrey Nyange “Kaburu” kushikiliwa na vyombo vya dola kutokana na kesi inayowakabili katika mahakama ya Kisutu, Simba wamejipanga na kupanga safu nzima ya mapambano wakati kesi dhidi ya Eveva ikiendelea.

Jumamosi Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ilikaa na kuamua mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ya uendeshaji wa klabu hiyo kubwa hapa nchini kwa mwaka huu.

Hata hivyo hata kabla ya kufanyika kwa kikao hicho baadhi ya viongozi walishagawana majukumu katika kuhakikisha kuwa Simba inasonga mbele.

Wanaoongoza mapambano hayo ni pamoja na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Zakaria Hans Poppe pamoja na mfadhili wa timu, Mohamed Dewji “MO” ambao ndio wanaoendeleza usajili ili kusuka kikosi kipya cha Simba. 

Licha ya vigogo hao wawili pia ndani ya jahazi hilo yumo mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji Musleh Al Rawah.

“Watatu hao ndio wamepewa dhamana ya kushusha vifaa vipya lakini pia kuna watu wengine wamekuwa msaada kwa Simba katika kipindi hiki,” amesema mtoa habari hizi.


“Watu wamekuwa na wasiwasi kuhusu viongozi wa Simba, nawahakikishia kuwa Simba ndio imekuwa imara. Unaju wakati wa matatizo watu wanasahau mpaka tofauti zao na kuwa kitu kimoja,” amesema.

No comments