INIESTA AMWAMBIA NEYMAR "USITUZOGOE BABA, TUCHANE TU KAMA UNABAKI AU UNASEPA ZAKO"

KIUNGO Andres Iniesta amevunja ukimya na kumtaka staa wa Brazil, Neymar, aamue moja mapema kama anabaki au anaondoka Barcelona.

Iniesta amesema kuwa, tetesi za kila siku zinazomwonyesha Neymar kutakiwa na PSG, zimekuwa zikiivuruga kambi yao, hivyo Mbrazil huyo atoke hadharani na kufanya maamuzi.

"Sote tunataka hili limalizike," alisema Iniesta, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari. "Lakini njia nzuri ya kulimaliza hili ni yeye kuzungumza.

"Tunapenda abaki na sisi, lakini pia tunataka hizi kelele zifike mwisho. Iwe kwa klabu kuzungumza na Neymar mwenyewe, naamini uamuzi wa hili ni faida kwa pande zote mbili."

Katika hatua nyingine, Neymar ameutaka uongozi wa Barca kuhakikisha wanambakisha nyota huyo, kwa kuwa hakuna fedha inayoweza kufikia uwezo wa Mbrazil huyo.

"Neymar ni miongoni mwa wachezaji bora duniani kwa sasa na ana faida kubwa kwetu," alisema. "Natumani ataendelea kuwa hapa kwa muda mrefu zaidi. Ni mawazo yangu tu.

"Sioni pauni milioni 200 au 300 zikiwa na faida kwa klabu kuliko kubaki naye. Nataka kucheza na wachezaji wa kiwango cha juu na Neymar ni mmoja wao."

Kauli hii ya Iniesta imekuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu Neymar alipopigana mazoezini na beki mpya wa Barca, Nelson Semedo.

Lakini Iniesta anaamini hali hiyo huwa inatokea mazoezini, japo si kawaida kuona matukio hayo yakitokea ndani ya Barcelona.

"Ni matukio ya kawaida kutokea wachezaji wakiwa mazoezi, japo kwetu huwa haitokei mara kwa mara,” alimaliza Iniesta.

No comments