JUMA LUZIO MBIIONI KUBAKI MSIMBAZI MSIMU UJAO

SIMBA inakaribia kumalizana tena na straika wa klabu ya Zesco United,  Juma Luzio ambaye aliitumikia katika Ligi Kuu msimu uliopita.

Habari za uhakika zinasema kwamba Simba wako katika mazungumzo na Luzio ili abaki Msimbazi kwa msimu mwingine kama hataki kurejea Zambia kuitumikia tena Zesco.

Luzio hajaongozana na wachezaji wengine wa Simba walioko katika kambi ya mazeozi nchini Afrika Kusaini ili kumalizana kwa mazungumzo na hasa ikizingatiwa kuwa mkataba ambao umemfanya acheze Simba umemalizika.

Hata hivyo habari zinasema kwamba tangu katikati ya wiki kumekuwa na mazungumzo kati ya pande zote na klabu hiyo ya Zambia iko tayari kuendelea kumwachia Luzio abaki Simba kwa miezi sita zaidi.

Simba walioondoka mwanzoni mwa wiki kwenda nchini huko na watakaa kwa siku 14 kabla hawajarejea nchini kwa ajili ya tamasha la Simba Day Agosti 8.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Luzio alisema mkataba wake wa mkopo ulishamalizika hivyo isingekuwa vyema kuondoka wakati wapo kwenye mazungumzo na viongozi wa Simba.

“Bado tupo kwenye mazungumzo na viongozi wa Simba kwa ajili ya kuingia mkataba mpya na tupo kwenye hatua za mwisho hivyo isingekuwa vizuri niondoke kabla ya kukamilisha jambo hili muhimu."


“Mungu akijalia basi msimu ujao nitakuwa hapa Simba, litakuwa jambo zuri kwa vile sasa nimezoeana na wenzangu, utakuwa wakati wa kuisaidia timu kufanya vizuri,” alisema Luzio ambaye hakuwa tayari kusema lini atasaini mkataba.

No comments