JUMA PONDAMALI AMWONYESHA KIPA DIDA KIDOLE CHA ONYO

JUMA Pondamali ambaye ni kocha wa makipa wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara, Yanga amemuonya mlinda mlango wao, Deogratius Munishi “Dida” kuwa anaweza kumsubiria yeye arudi toka kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Pondamali maarufu kwa jina la Mensah alisisitiza kuwa klabu ya Yanga itaendelea na mipango yake ya usajili na kutengeneza kikosi chake pasipo kusubiria ratiba za mchezaji yoyote ambaye yuko nje ya kikosi kwa sasa.

“Tunajua shauku ya Dida kutaka kucheza soka nje ya nchi, lakini kamwe sisi hatuwezi kusimamisha mipango ya timu kwa sababu ya ndoto za mtu mmoja,” alisema Pondamali.

“Kipa tuliyempata kutoka African Lyon anatutosha wakati huu kwani tumeridhika na uwezo wake baada ya kumuona uwanjani msimu uliopita, hivyo Dida akae akijua kuna hilo linaendelea hapa jangwani,” aliongeza.


Yanga imeendelea na mipango yake ya usajili wa kimyakimya, huku Dida ambaye mkataba wake umefika tamati akiwa na shauku ya kutaka kucheza soka nje ya mipaka ya Tanzania, jambo linaloweza kumletea ukakasi wa namba ikiwa hatafanikiwa kwenye hatua za majaribio.

No comments