KAGERA SUGAR YAANZA KUJIFUA "KIJESHI" KWA AJILI LIGI KUU MSIMU UJAO

KIKOSI cha Kagera Sugar kimekuwa cha kwanza kufunga zoezi la usajili na kimeanza maandalizi ya kufa mtu kujiwinda na Ligi Kuu msimu ujao.

Kagera Sugar kwa sasa inajifua kwenye uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam kabla ya wiki ijayo kwenda kuweka kambi ya kudumu mkoani Kagera.

Akiongea na saluti5, kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime kwa sasa amefunga zoezi la usajili na kuelekeza akili kwenye maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Alisema, baada ya kurudi Kagera wataendelea na program yao ya mazoezi sambamba na kujipima ubavu na baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu pamoja na mechi za kirafiki na timu kutoka nje ya nchi.

“Zoezi la usajili tumelifunga rasmi na hatutaongeza wala kupunguza mchezaji yeyote, kwa sasa kikosi kimekamilika na tunafanya mazoezi kwenye uwanja wa Karume na baada ya wiki moja tutarejea kwenye kambi yetu ya Kagera kuendelea na ratiba zetu,” alisema Maxime.


Kagera ambayo inaongozwa na nyota wakongwe Juma Kaseja pamoja na Juma Nyoso, msimu uliopita iliweza kufanya vyema na kujikuta ikikamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

No comments