KANU NWANKWO KUJENGA HOSPITALI KWA AJILI YA KUMUENZI TIOTE

MCHEZAJI nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Kanu Nwankwo amesema kifo cha hivi karibuni cha mchezaji mashuhuri wa Ivory Coast, Cheick Tiote kinafaa kuwa “funzo” na kuhakikisha hatua zinachukuliwa kuhusu maradhi ya moyo barani Afrika.

Tiote akiwa na miaka 30, alifariki mapema mwezi uliopita baada ya kuzirai wakati akifanya mazoezi uwanjani nchini China ambako alikuwa anachezea klabu ya Ligi daraja la pili ya Beijing Enterprises.

Kanu ambaye nae pia alikabiliana na matatizo ya moyo wakati wa uchezaji wake, amesema wakati umefika kwa hatua kuchukuliwa kuhusu maradhi ya moyo uwanjani na nje ya uwanja.

Mchezaji huyo wa Nigeria aliacha kucheza kwa miezi tisa, baada ya madaktari kugundua kasoro kwenye moyo wake wakati akiwa katika timu ya Inter Milan.

Ilikuwa ni miezi kadhaa baada ya kulisaidia taifa lake kushinda dhahabu katika michezo ya Olimpiki 1996 mjini Atlanta.

Hata hivyo, aliweza kurejea uchezaji wake baada ya kufanyiwa upasuaji nchini Ohio, Marekani.

“Kifo cha Tiote hakikuwa habari nzuri. Haikuwa mara ya kwanza kwa hilo kutokea,” alisema Kanu na kuongeza:
“Tulimpoteza Marc-Vivien Foe. Alifariki dunia lakini hakuna lililofanywa.”

Tiote amejiunga na orodha ndefu ya wachezaji wa Afrika ambao wamefariki uwanjani kutokana na maradhi ya moyo.

Lakini kanu, mchezaji wa zamani wa Ajax Amsterdam, Inter Milan, Arsenal na Portsmouth FC, anasema atachangia kukabiliana na tatizo hilo.

Anapanga kujenga hospitali ya moyo yenye thamani ya dola mil 17 mjini Abuja, Nigeria. Anataka pia kujenga hospitali nyingine kama hiyo katika nchini nyingine moja ya Afrika Mashariki, Kaskazini na Kusini mwa Afrika.

“Nazungumza na marafiki ili tufanye jambo, tuwahamasishe watu, tujaribu kuwasaidia watoto Afrika,” anasema Kanu.


“Mtu mmoja hawezi kufanya kila kitu. Kilichomtokea Tiote ni funzo kwetu sote. Hatuwezi kuruhusu mambo yaendelee hivi. 

Lazima tulizungumzie. Lazima tuzungumze zaidi kuhusu hili, habari zinafaa kusambazwa kwa sababu tatizo hili ni kubwa.”

No comments