KIUNGO HATARI WA APR YA RWANDA AJIPELEKA SIMBA SC

KUNA habari njema ambayo wana Simba wanaweza kuifurahia kama wataisikia kupitia saluti5.

Habari yenyewe njema ni hii kauli ya kiungo hatari wa timu ya maafande wa jeshi la Rwanda, APR Jean Claud Iranzi ambaye amejiweka sokoni kwa ajili ya soka la Simba.

Taarifa kutoka kwa rafiki wa karibu na kiungo huyo na kutua katika dawati la michezo la mtandao huu zinasema Iranzi ameweka bayana azma yake ya kutaka kusakata soka nchini Tanzania lakini akaitaja Simba kuwa ni timu anayodhani inaweza kuanzisha mazungumzo naye.

Kwa mujibu wa rafiki yake huyo anayeishi jijini Dar es Salaam, ameieleza saluti5 kuwa Iranzi amefunguka na kutaja nia yake ya kuja kucheza soka Tanzania lakini kama timu ya kujiunga nayo anapenda atue kwa wana Msimbazi.

“Jean amevutiwa na sera ya Simba ya kuwa wepesi wa kuruhusu wachezaji pindi wanapopata nafasi za timu za nje.”

“Lakini pia Jean amekuwa akifuatilia mno timu za Tanzania na kukiangalia kikosi cha Simba na kubaini kuwa pindi akijiunga ana uhakika wa kupambana kwa ajili ya kupata nafasi katika kikosi cha kwanza.”


“Kutokana na hili ni kama amefungua milango kwa klabu ya Simba kuanza mazungumzo na kiungo huyo hasa katika kipindi hiki kwa kufunguliwa kwa dirisha la usajili,” alizungumza rafiki huyo wa Iranzi ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu maalum.

No comments